Watumishi waliotajwa kashfa ya escrow wako kazini
Dar es Salaam. Watumishi wawili wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), waliotajwa katika kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow wanaendelea na kazi wakisubiri taratibu za utumishi wa umma kabla ya kuchukuliwa hatua.
Akizungumza na mwandishi wetu kuhusu hatua
zilizochukuliwa baada ya agizo la Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba
kutaka wafukuzwe, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi, Richard
Kayombo alisema jana kwamba hawajachukuliwa hatua hadi taarifa za
uchunguzi za vyombo vya dola itakapotolewa.
Watumishi wawili, mmoja alitajwa katika taarifa ya
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), kutokana na matokeo ya
ukaguzi maalumu wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),
kuhusu kashfa hiyo kwamba aliingiziwa Sh1.6 bilioni bila maelezo.
Mwingine katika kashfa hiyo, badala ya kuandika
Dola za Marekani 6 milioni aliandika Sh6 milioni na badala ya kuandika
Dola za Marekani 20 milioni, aliandika Sh20 milioni.
Kutokana na taarifa hizo wakati wa mkutano wa
Bunge wa 16 na 17 uliomalizika hivi karibuni, Mwigulu aliagiza mtumishi
wa mamlaka hiyo aliyepata mgawo wa Sh1.6 bilioni kutoka katika Akaunti
ya Tegeta Escrow afukuzwe kazi jamba ambalo TRA imesema litatekelezwa
baada ya vyombo vya dola kufanya uchunguzi.
Jana, Mwigulu alisema kuwa Kamishna wa TRA
amemweleza kuwa kinachofanyika hivi sasa ni kufuata taratibu za utumishi
wa umma ili kuwapa watumishi hao nafasi ya kujieleza.
Alisema kutokana na hali hiyo pamoja na taratibu hizo kufuatwa watafikia tu katika maagizo yake aliyoyatoa bungeni.
Akizungumzia agizo lake kwa wale ambao walipata
mgawo wa escrow kuwataka walipe kodi kabla ya kufika Desemba 31 mwaka
huu, Mwigulu alisema msimamo wa Serikali uko palepale kwamba wasipofanya
hivyo watachukuliwa hatua kali.
“Nimezungumza na Kamishna wa TRA leo (jana)
amenieleza watawapelekea fomu za kodi wajaze kwa ajili ya kulipa, hivyo
msimamo uko palepale kwamba watalipa hiyo kodi,” alisema Mwigulu.
chanzo:mwananchi
chanzo:mwananchi
Comments
Post a Comment