Vyama vya Chadema na CCM vimeingia katika mchuano wa kuwania nafasi ya kurusha matangazo ya moja kwa moja ya kampeni za wagombea urais katika televisheni Jumamosi hii. Wakati Chadema ikitaka muda wa kurusha matangazo ya uzinduzi wa kampeni za mgombea wake, Edward Lowassa kutokea jijini Dar es Salaam, CCM inataka kurusha matangazo ya mkutano wa kampeni ya mgombea wake, Dk John Magufuli kutoka jijini Mbeya. Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene alisema jana kuwa kumekuwa na njama za CCM kutaka kuzuia fursa ya Chadema kurusha kampeni za mgombea wake kwa kutaka siku hiyo irushe kampeni za Dk Magufuli. Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alikiri chama hicho kutaka kurusha matangazo ya mgombea wake na kuhoji; “tatizo liko wapi kama Chadema imechelewa kulipia?” “Ni kweli mgombea wetu wa urais akiwa Mbeya tutarusha matangazo ya kampeni zake moja kwa moja kwenye runinga, sasa ni runinga ngapi siwezi kujua maana kuna watu wanalifanyika kazi suala hilo. Lakini kama...