sakata la Escrow Wabunge waungana

BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jana lilikuwa moja dhidi ya utoaji wa fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), huku baadhi ya mawaziri wakitofautiana na taarifa ya Serikali ya utetezi wa suala hilo.

Kabla ya kuungana huko kwa wabunge, Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha za Serikali (PAC), Kabwe Zitto alihitimisha hoja ya kamati hiyo na Bunge kuingia katika hatua ya kufanya uamuzi wa maazimio ya Bunge dhidi ya watuhumiwa wa uchukuaji wa fedha hizo.

Awali kabla ya kufikia hatua ya maazimio, ambayo iliendelea mpaka jana usiku, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba alikiri kuwa katika fedha zilizochotwa katika akaunti ya Tegeta Escrow katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kuna kodi ya Serikali na aliagiza wote walionufaika na fedha hizo kulipia kodi ifikapo Desemba 31, mwaka huu.

Alisema Serikali ilipaswa kulipwa Sh bilioni 26.97, lakini hadi sasa imelipwa Sh bilioni 4.21.
Akichangia mjadala kuhusu taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), kuhusu matokeo ya ukaguzi maalumu wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika akaunti ya Tegeta Escrow, mali ya wanahisa wa Kampuni ya Kufua Umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL).

Naibu Waziri huyo ambaye mchango wake ulipongezwa na wabunge wengine waliozungumza baada ya yeye, alisema kimsingi Serikali ilipaswa kukusanya kodi yake katika fedha hizo Sh bilioni 306, lakini kodi imekokotolewa kizembe na hivyo kuinyima mapato zaidi Serikali. “Katika hili la fedha, tayari uchunguzi unaendelea …kazi inaendelea.

Kwa upande wa kodi, kuna mambo matatu yalipaswa kufanyika. VAT (Kodi ya Ongezeko la Thamani) ilipaswa kukokotolewa kutoka katika chanzo, na hili lingefanyika, tusingeongelea hapa leo. Niwatangazie Watanzania kuwa jambo hilo linashughulikiwa na tunapaswa kupata kodi ya Sh bilioni 26.97,” alisema.
Akishangiliwa na wabunge, Naibu Waziri aliongeza: “Baada ya kugundua kuwa haijakusanywa kodi hiyo, kazi ilianza na hivi sasa tumelipwa Sh bilioni 4.21 kutoka katika akaunti ya Escrow. Fedha iliyobaki italipwa, lazima italipwa. Hatuwezi kuacha kodi kubwa namna hii kwa tajiri, halafu tunafukuzana na mama muuza nyanya barabarani.”

Alisema iligundulika kuwa suala hilo lilikosewa katika kukokotoa hesabu za kodi na TRA imechukua hatua kwa kumuandikia barua mhusika (mmiliki wa PAP, Harbinder Singh Sethi) ya Novemba 19, mwaka huu, ya kusudio la kufuta cheti cha capital gain tax.

Pia alisema juzi Novemba 27, mwaka huu, Wakala wa Usajili wa Makampuni (BRELA), wamepewa notisi kuhusu kuchukua fedha zaidi katika suala la uhamishaji wa hisa za kampuni hiyo.
Waliovuna VIP

Kuhusu watu mbalimbali waliofaidika na fedha hizo kutoka kwa mmiliki wa Kampuni ya VIP Engineering, James Rugemalira aliyepata Sh bilioni 75, Naibu Waziri wa Fedha alisema wanapaswa kulipa kodi ya Serikali, hivyo hadi kufikia Desemba 31, mwaka huu, wawe wamefanya hivyo.
“Bunge lako Mheshimiwa Mwenyekiti lisihangaike, wale wote waliofaidika na fedha hizi, wajiandae kisaikolojia. Hili ni jambo la kimaadili, wale wote waliopokea fedha hizo, wanapaswa kulipa kodi. Hadi kufikia Desemba 31, wawe wamelipa kodi, baada ya hapo, TRA itawashukia,” alisema Mwigulu na kushangiliwa na wabunge wengi.

Aidha, alisema kwa mujibu wa taarifa za watendaji wa benki mbili za Stanbic na Mkombozi zilizotumika kugawa fedha kwa watu mbalimbali, si kweli kuwa zilichukuliwa kwenye mifuko ya rambo, sandarusi au viroba kama ilivyodaiwa na taarifa ya PAC, bali walilipwa kwa hundi kama ambavyo taratibu zinavyoeleza zinapozidi Sh milioni 10.

Lakini aliwaagiza watendaji wa benki hizo, kufikia muda wa kazi jana, wawe wametoa taarifa kuhusu taratibu zilizotumika katika kutoa fedha hizo, ili kuwaondolea wasiwasi wateja wake na umma kwa ujumla, akisema wana haki ya kujua na kwamba wakati mwingine kukaa kimya bila kueleza upande mwingine, kunasababisha kutolewa taarifa potofu.
Hatua

Akiwarudia watendaji wa Serikali waliohusika katika kashfa hiyo, aliwaambia wabunge kuwa jambo wanalosubiri wananchi si kuongea, bali ni kuchukua hatua, hivyo wote waliohusika na hilo wanapaswa kuwajibika.
“Sisi hapa hatuna namna ya kushughulikia wanasiasa. Nimewahi kusema kwamba mtu anapoiba na kujiuzulu haisaidii, watendaji na wataalamu hawawajibiki popote… anajiuzulu mtu lakini hasara zilizopatikana hazirudi,” alisema Mwigulu kabla ya kukatishwa na kengele ya kumaliza muda wakati akitoa ushauri wa nini kifanyike watendaji hao.
Wabunge wengine

Katika michango yao, wabunge wengine jana waliendelea kumtetea Waziri Mkuu Mizengo Pinda, kwamba hahusiki na sakata hilo, lakini wakataka wengine waliohusika wawajibike wenyewe au waondolewe katika nyadhifa zao na wasionewe huruma.

Mbunge wa Kishapu, Suleiman Nchambi (CCM), akitumia nukuu za Biblia na Kurani, alimtetea Waziri Mkuu Pinda, na kumtuhumu Zitto kutumia nafasi yake ya uenyekiti wa PAC kuchukua fedha kwa ajili ya kampuni zake binafsi kutoka katika mashirika anayoyasimia.

Mbunge wa Mkanyageni, Mohammed Habib Mnyaa (CUF), alilitaka Bunge kusimamia ukweli na kuhoji kwa nini hadi leo maazimio ya sakata la Richmond hayajafanyiwa kazi, kwani yangeepusha kutokea kwa sakata hili la Tegeta Escrow.
Naye Mbunge wa Gando, Khalifa Suleiman Khalifa (CUF), alisema sakata hilo linaonesha kuwa kuna mazingira ya udanganyifu, na kuongeza kuwa uwajibikaji ni lazima na wananyooshewa vidole, wanapaswa kuchukua hatua.

Mbunge wa Nkenge, Assumpter Mshama (CCM), licha ya kutakiwa kuomba radhi baada ya kudai Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, amefaidika na fedha hizo za Escrow, alitaka wahusika wanaotajwa katika sakata hilo, wajipime wenyewe.

Kauli yake iliungwa mkono na Mbunge wa Sikonge, Said Mkumba (CCM), na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia, ambao walisema si vyema kuchanganya watu wengine katika sakata hilo, bali wahusika ndio wabebe misalaba yao.

Ghasia pia aliitaka PAC itaje watu ambao waligawana fedha katika mifuko ya sandarusi na viroba kama ilivyodai. Aidha, Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka (CCM), yeye ‘alikufa’ na watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini, kuanzia Waziri Profesa Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wake, Eliachim Maswi na kusisitiza wawajibike, akisema “watu waligawana fedha kama chakula cha njaa.”

Kangi Lugola (Mwibara – CCM), James Mbatia (Kuteuliwa – NCCRMageuzi) na Michael Laizer (Longido – CCM), wote walisisitiza kuwajibika kwa waliohusika na kashfa hiyo, wakati Mbunge wa Mbozi Magharibi, David Silinde (Chadema), alisema wabunge wamekuwa wajasiriamali wanaotetea wezi.
Mjadala huo kuhusu taarifa ya PAC juu ya Tegeta Escrow ulitarajiwa kufungwa jana jioni kwa Bunge kupitisha maazimio na kisha kuahirishwa.
Mwandosya

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, asiye na Wizara Maalumu, Profesa Mark Mwandosya, alisema fedha hizo ni za umma kwa kuwa zilikuwa katika akaunti ya BoT, ambayo ni benki ya umma.
Alisema hata vitabu vya kumbukumbu vya BoT, vilikuwa vikieleza kuwa fedha hiyo ni ya umma ndio maana hata Gavana wa benki hiyo, Profesa Beno Ndulu, alilazimika kuwa na wasiwasi wakati wa kuidhinisha fedha hiyo.
Wassira
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Uhusiano na Uratibu, Stephen Wassira, alisema ni bora kuwa masikini na kuheshimika kuliko kutetea sakata hilo.
Alitaka wote wanaohusika wachukuliwe hatua huku akisisitiza hata CCM haiwezi kukubaliana na hilo kwa kuwa hakuna chama cha wezi, ila ndani ya vyama kuna wezi.

Comments

Popular posts from this blog

hii ni list ya baadhi ya majina ya wasanii wa Nigeria waliohit mwaka huu kuanzia A-Z

mbinu za kuwa producer au mtayarishaji wa music